Sababu na matibabu ya tatizo la kujamba kwa Uke
Hii ni hali ya utoaji wa hewa au gesi uliyojikusanya ndani ya Uke.
Tofauti na kujamba kwa kawaida ambako hutokea kwenye tundu la haja kubwa, uke huwa hautoi gesi chafu ambazo hutoa harufu kali.
Kitendo hiki kinaweza kutokea wakati wa tendo la ndoa, mazoezi au pale ambapo mwanamke anakuwa anafanya kazi zozote ngumu.
Katika mazingira ya kawaida, jambo hili huwa halina maana mbaya kwa afya, na halijaanza kutokea kwako.
Chanzo
Najua unataka kufahamu nini hasa husababisha kutokea kwa changamoto hii ambayo huwafanya wanawake wengi wapunguze kujiamini.
Twende pamoja.
1. Ngono
Tendo la ndoa ndiyo chanzo kikubwa kinachofanya gesi ijikusanye kwenye uke.
Kitendo cha kuingia na kutoka kwa uume kunaweza kufanya gesi ijikusanye ndani.
Inapotokea mwanamke kafika kileleni, au mwanamme anapotoa uume wake, gesi hii hutolewa nje ya uke kwa kutoa sauti kubwa.
Kitendo cha mwanamke kutumia vidole vyake au kuingiza vifaa vingine vyenye uke kwa lengo la kujisisimua mwenyewe kunaweza pia kusababisha kutokea kwa changamoto hii.
2. Mazoezi
Ushiriki wa mazoezi magumu kunaweza kusababisha kuingia kwa gesi kwenye uke.
Baadhi ya wanawake huripoti kuwa wanapokuwa wanafanya mazoezi hasa yale ya yoga hukumbwa na hali hii.
3. Misuli ya nyonga
Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa kujamba kwa uke huwa ni dalili muhimu sana inayoweza kutumika kuonesha uwepo wa changamoto kwenye misuli ya sakafu ya nyonga.
Hii inaweza kuwa hivyo tangu kuzaliwa, au inaweza kutokea wakati wowote baada ya kuzaliwa.
4. Fistula
Ni uwepo wa tundu la wazi kati ya uke na sehemu zingine za ndani ya mwili wa mwanamke.
Fistula inaweza pia kusababisha kujaa kwa hewa kwenye uke, hivyo kuwa chanzo cha tatizo hili.
Tiba
Kujamba kwa uke hudumu kwa sekunde chache tu, ni tendo la kawaida ambalo mara nyingi huwa halina maana mbaya kwa afya.
Hakuna tiba ya moja kwa moja ya changamoto hii kwa kuwa huisha yenyewe tu baada ya muda fulani. Ikiwa kujamba kwa uke kunasababishwa na uwepo wa tatizo au ugonjwa mwingine, mwanamke atachunguzwa na kutubiwa kikamilifu.
Dawa, baadhi ya mazoezi hasa yale ya kegel au upasuaji unaweza kufanyika ili kutibu changamoto hii.
Tahadhari
Jambo hili husumbua, huondoa kujiamini na linaweza kuleta sintofahamu kubwa kwenye uhusiano.
Lakini, nataka nikuhakikishie kuwa ni jambo la kawaida na halina maana yoyote mbaya kwa afya. Ni asilimia ndogo sana ya wanawake huwa na matatizo mengine ambayo huonekana kwao kupitia dalili hii.
Ni changamoto inayopona yenyewe tu baada ya muda fulani.
Hata hivyo, ikiwa inatokea wakati ambao haushiriki tendo la ndoa ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya yako